
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema yuko tayari kushiriki mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ikiwa hatua hiyo itasaidia kufanikisha jitihada za amani.
Akizungumza baada ya mkutano wake na Rais wa Marekani, Donald Trump, Zelensky alisema bado hakuna tarehe iliyowekwa kwa mazungumzo hayo, lakini alithibitisha kuwa pande zote mbili zimeonesha nia ya kuendelea na mazungumzo.
“Imethibitishwa kwamba wako tayari kwa mkutano wa pande tatu,” alisema Zelensky. “Ikiwa Urusi ilipendekeza kwa rais wa Marekani mkutano wa kidiplomasia kati ya pande zinazowakilisha nchi mbili, pia tutaona matokeo yake. Ukraine haitakuwa kikwazo cha kufikia amani.”
Kauli hiyo ya Zelensky inakuja muda mfupi baada ya Trump kumpigia simu Putin wakati mkutano wa White House ukiendelea. Kupitia taarifa yake, Trump alisema:
“Nilimpigia simu Rais Putin na kuanza maandalizi ya mkutano katika eneo litakaloamuliwa kati ya marais Putin na Zelensky. Baada ya mkutano huo, tutakuwa na mkutano wa pande tatu, ambao utajumuisha Marais wawili pamoja na mimi mwenyewe.”
Aidha, Trump alibainisha kuwa suala la usalama wa Ukraine limepata msisitizo mpya, akisema Ulaya imekubali kushirikiana na Marekani kutoa dhamana za kiusalama kwa taifa hilo.
“Dhamana ya usalama kwa Ukraine itatolewa na nchi mbalimbali za Ulaya, kwa uratibu na Marekani,” alisema Trump.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!