Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Umoja Wa Mataifa Walitunukia  Jwtz Nishani Ya Ulinzj Wa Amani Nchini Jamhuri  Ya Afrika Ya Kati

  • 4
Scroll Down To Discover

Kikosi Cha Nane cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TANBAT 08), kinacholinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kimetunukiwa  Nishani za Ulinzi wa Amani na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na mchango wake mkubwa katika operesheni ya kulinda amani nchini humo chini ya mwavuli wa MINUSCA.
Katika sherehe ya gwaride la heshima iliyofanyika tarehe 06 Septemba 2025 mjini Berberati, wanajeshi zaidi ya 500 wa TANBAT 08 wametunukiwa nishani hizo ikiwa ni ishara ya kutambua michango yao  katika kuwalinda raia, kusaidia shughuli za kibinadamu, na kuimarisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.
Uvishwaji wa nishani hizo uliongozwa na  Naibu Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa nchini CAR,  Meja Jenerali Maychel Asmi, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Katika hotuba yake, Meja Jenerali Asmi ametoa pongezi kwa uongozi, nidhamu na mshikamano mkubwa uliodhihirishwa na TANBAT 08 wakati wa operesheni zao.
 “Wanajeshi wa JWTZ wametoa mchango mkubwa sio tu katika kulinda amani, bali katika kujenga uhusiano mzuri na jamii kwa ujumla. Huu ni mfano wa kuigwa na vikosi vingine,” alisema Meja Jenerali Asmi.
Naye Kamanda wa TANBAT 08, Luteni Kanali Theofil Nguruwe, amesema kuwa kutunukiwa nishani hizo ni ushahidi wa uaminifu, juhudi na uzalendo wa wanajeshi wake katika kutimiza majukumu ya kimataifa.
 “Tumehudumu kwa weledi, heshima na moyo wa kizalendo. Hii ni heshima kwa JWTZ na kwa taifa letu la Tanzania,” alisema Luteni Kanali Nguruwe.
Sherehe hiyo  imepambwa na maonesho kabambe ya kareti kutoka kikundi maalum cha makomando wa JWTZ  pamoja na burudani ya ngoma za utamaduni wa Kitanzania kutoka kikundi cha sanaa cha JWTZ, ngoma zilizowakilisha utambulisho na mshikamano wa taifa la Tanzania  jambo lililopokelewa kwa shangwe na wageni mbalimbali.
Sherehe hiyo pia imehudhuriwa na Maafisa Waandamizi wa MINUSCA, Maafisa Wanadhimu kutoka Makao Makuu ya JWTZ,  viongozi wa Serikali ya CAR, Mashirika ya Misaada ya Kibinadamu pamoja na wananchi wa Berberati  ambao waliwapongeza wanajeshi wa Tanzania kwa kazi yao ya kujitoa kwa ajili ya amani ya nchi yao.
Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa kutoa vikosi bora vya ulinzi wa amani na kufanya vizuri kwa zaidi ya miaka 30 ya kushiriki katika operesheni mbalimbali duniani.



Prev Post TOTALENERGIES YAZINDUA KITUO CHA KWANZA CHA HUDUMA KIMARA, DAR ES SALAAM
Next Post ‎BENKI YA USHIRIKA YAZIDI KUPANUA WIGO WA HUDUMA ZA KIFEDHA NCHINI
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook