
Dar es Salaam – Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema chama hicho kimepanga kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masijala Ndogo Dar es Salaam, wa kutupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ya kuondoa ushahidi wa mashahidi wa siri katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo.
Mnyika amesema CHADEMA haitaridhika na uamuzi huo, ikiamini kuwa si sahihi kisheria, na kwamba wataendelea kushauriana na Lissu ili kuwasilisha rufaa rasmi kupinga maamuzi hayo.
“Tunadhani huu uamuzi si sahihi. Tutakaa na Mwenyekiti wetu, Tundu Lissu, kupanga hatua za kisheria, ikiwemo rufaa,” alisema Mnyika.
Aidha, aliwataka wanachama wa chama hicho kubaki watulivu na kuendelea kujenga chama katika maeneo yao, akisisitiza mshikamano wa ndani wakati mchakato wa kisheria ukiendelea.
Kesi hiyo, inayomkabili Lissu, imekuwa gumzo kwa mjadala mpana kuhusu matumizi ya mashahidi wa siri katika mashauri ya jinai na athari zake kwa haki ya mtuhumiwa kusikilizwa kwa usawa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!