Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Safari ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Tanzania si jambo lililoanza mwaka 2016 wala mwaka 2018, ina historia ya zaidi ya nusu karne, ikianzia katika uamuzi wa Chama cha TANU mwaka 1973 wa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.
Miaka iliyofuata iliendelea kuwa ya maandalizi na utekelezaji wa hatua mbalimbali, hadi Serikali ilipokuja kutoa msukumo mpya mwaka 2016 na hatimaye kuanza kujenga Mji wa Serikali Mtumba kwa awamu.
Mwaka 1973, Halmashauri Kuu ya Chama cha TANU ilikaa Dar es Salaam na kuridhia kwamba Makao Makuu ya nchi yawe Dodoma.
Uamuzi huo uliweka msingi wa safari ndefu ya kuhamisha shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ambayo utekelezaji wake uliendelea kwa hatua mbalimbali katika Serikali zilizofuata.
Katika miaka iliyofuata, Serikali iliendelea kutekeleza hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na taasisi muhimu.
Ujenzi wa Bunge Dodoma na kuhamishiwa kwa shughuli za Bunge mjini humo ulikuwa miongoni mwa hatua hizo, huku Ikulu ya Chamwino pia ikiwa sehemu ya maandalizi ya muda mrefu ya kuimarisha Dodoma kama Makao Makuu.
Hivyo, uhamishaji wa Serikali haukuwa jambo jipya lililoanzishwa mwaka 2016, bali ulikuwa mwendelezo wa mpango uliokuwepo tangu mwaka 1973.
Mwaka 2016 ukawa hatua muhimu katika historia hiyo baada ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza rasmi mpango wa kuhamishia shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Serikali ilieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa utekelezaji wa ahadi ya Baba wa Taifa ya mwaka 1973.
Tarehe 23 Julai 2016 Rais Magufuli alitangaza Serikali kuhamia Dodoma na baadaye tarehe 25 Julai 2016 akasisitiza mpango huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika Dodoma.
Baada ya uamuzi huo, zoezi la kuhamisha shughuli za Serikali lilianza kutekelezwa kwa kasi.
Kufikia Aprili 2018, zaidi ya watumishi 3,800 walikuwa tayari wamehamia Dodoma, huku Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Rais zikiwa zimehamia mjini humo.
Serikali pia iliendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu iliyolenga kuwezesha Dodoma kubeba majukumu ya Makao Makuu ya nchi.
Katika hatua hiyo ndipo eneo la Mtumba likaanza kupata sura mpya kama kituo maalumu cha shughuli za Serikali.
Ujenzi wa awamu ya kwanza wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza tarehe 28 Novemba 2018, ukiwa na majengo 23 ya ofisi za muda.
Majengo hayo yalikamilika tarehe 22 Machi 2019 na kuwezesha baadhi ya watumishi wa wizara na taasisi kuanza kuhamia Mtumba wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya ujenzi wa majengo ya kudumu.
Baada ya awamu hiyo ya kwanza, Serikali iliingia katika hatua kubwa zaidi ya kujenga Mji wa Serikali wa kudumu. Awamu ya pili ilianza Oktoba 2021 na ilihusisha ujenzi wa majengo ya kudumu kwa ajili ya wizara na taasisi zilizopangwa kuhamia Mtumba, pamoja na miundombinu mbalimbali ya huduma.
Hatua hiyo ndiyo iliyoanza kubadilisha kwa kasi sura ya Mtumba kutoka eneo la majengo ya muda kwenda kuwa mji wa kisasa wa shughuli za Serikali.
Ujenzi uliendelea katika miaka iliyofuata sambamba na kuongezeka kwa idadi ya taasisi na watumishi waliokuwa wakihamia Dodoma.
Miundombinu iliyojengwa haikuhusu majengo pekee, bali pia barabara za lami, mifumo ya mawasiliano, TEHAMA, maji safi na majitaka, umeme, usalama na huduma nyingine muhimu.
Serikali pia ilianza kuweka miundombinu ya umeme chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42, pamoja na mifumo ya CCTV na kituo cha zimamoto.
Kufikia mwaka 2026, Mji wa Serikali Mtumba ulikuwa umefikia hatua kubwa ya utekelezaji. Mpango wa uzinduzi ulihusisha majengo ya ofisi za wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 59.1.
Majengo hayo yamepangwa kutoa mazingira ya kisasa ya kazi kwa takribani watumishi 18,510.
Katika hatua hiyo, Serikali pia imeendelea kuhamisha watumishi na taasisi kwenda Mtumba kwa awamu kadiri majengo yanavyokamilika. Mji huo sasa si eneo la ujenzi pekee, bali umeanza kufanya kazi kama kituo cha shughuli za Serikali, huku uwepo wa wizara na taasisi katika eneo moja ukilenga kurahisisha uratibu, mawasiliano na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Taarifa ya Serikali ya Oktoba 25, 2026 inaeleza kuwa ujenzi wa majengo ya kisasa ya wizara na taasisi ulianza mwaka 2021 na Serikali imewekeza takribani Sh bilioni 700 katika ujenzi wa Mji wa Serikali.
Pia, umewekewa mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha taasisi kuwasiliana na kutekeleza majukumu kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kupunguza urasimu na muda wa kushughulikia nyaraka.
Sasa, baada ya historia ndefu iliyoanzia kwenye uamuzi wa TANU mwaka 1973, kuendelea kwa maandalizi katika Serikali zilizofuata, msukumo mpya wa mwaka 2016 na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulioanza kwa awamu mwaka 2018, safari hiyo inafikia hatua nyingine muhimu. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Oktoba 2026.
Akizungumza Oktoba 27, 2026 jijini Dodoma kuelekea uzinduzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, alieleza uzinduzi wa miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Kabudi alibainisha awamu ya kwanza ya ujenzi ilianza Novemba 28, 2018 na ilihusisha majengo 23 ya ofisi za muda, huku awamu ya pili iliyoanza Oktoba 2021 ikihusisha majengo ya kudumu na miundombinu mbalimbali.
Amebainisha kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaimarisha uratibu wa shughuli za Serikali na kurahisisha mawasiliano baina ya wizara na taasisi.
Aliongeza Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya Mji wa Serikali na Dodoma kwa ujumla, huku akibainisha kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kutasaidia kuongeza idadi ya watu wanaofika Dodoma na hivyo kuongeza fursa za kiuchumi.
Aidha, Prof. Kabudi amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali kutumia vizuri miundombinu hiyo na kuhakikisha mazingira hayo yanaimarisha uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akisisitiza kuwa majengo mazuri pekee hayatoshi bila utendaji bora na nidhamu ya kazi.












Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!