
Ajira, ujuzi wa ufundi na kuimarika kwa biashara ndogo ni miongoni mwa fursa ambazo wananchi wameanza kupata kutokana na ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, ambao umefikia asilimia 78.
Baadhi ya vijana wanaoshiriki ujenzi huo wamesema wamepata kipato cha kuendesha familia zao, huku wengine wakijifunza stadi zinazoweza kuwawezesha kujiajiri baada ya mradi kukamilika. Waliyasema hayo walipozungumza na waandishi wa habari.

Mhandisi Msimamizi wa Mradi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), John Paul, anasema eneo la Mbamba Bay lilichaguliwa baada ya upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2023 kubaini umuhimu wake katika kuimarisha huduma za bandari.
Mhandisi huyo anasema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri kutokana na usaidizi wa Serikali na upatikanaji wa fedha zinazomwezesha mkandarasi kulipwa kwa wakati:”Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na kutoa fedha kwa wakati,” anasema Paul.

Amepongeza Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili malengo yaliyowekwa na Serikali yafikiwe na kusaidia bandari hiyo na nyingine kukua zaidi.
Naye Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Anova, Agathon Mwenda, anasema kazi zinaendelea vizuri na wana dhamira ya kukamilisha ujenzi huo ifikapo Februari 26, 2027, kwa mujibu wa mkataba.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) unatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa mizigo na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.
The post Ujenzi Bandari Mbamba Bay Waanza Kuwanufaisha Wananchi appeared first on Global Publishers.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!