
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewakamata watu wawili akiwemo Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika, Ferdinand Anthony maarufu kama Masembo, na raia mwingine Hussein Ally maarufu kama Madebe, kwa tuhuma za kushiriki kumpiga hadi kifo Enock Thomas Mhangwa, wakimtuhumu kwa kosa la wizi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, tukio hilo linahusishwa na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ambapo watuhumiwa walimshambulia marehemu kwa kipigo kikali hadi kusababisha kifo chake. Jeshi la Polisi limesema bado linaendelea na msako mkali kuwasaka watuhumiwa wengine waliotoroka, akiwemo Afisa Mtendaji wa Kata ya Uyovu na Mgambo wawili wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika pale panapotokea tuhuma au uhalifu wa aina yoyote.
“Hili ni tukio la kusikitisha, hatutavumilia watu kuchukua sheria mikononi mwao. Tunawasaka wote waliohusika,” alisema Kamanda huyo.
Mwili wa marehemu Enock Thomas Mhangwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya kwa uchunguzi zaidi huku uchunguzi wa kina ukiendelea.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!