
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuungana, kushikamana na kushirikiana kwa lengo la kuharakisha maendeleo, huku akisisitiza kuweka kando tofauti za kikabila, kidini na kisiasa.
Shigongo alitoa kauli hiyo Julai 2, 2025 wakati wa hafla ya mapokezi ya kivuko cha MV Mwanza, kilichopokelewa kwa shangwe katika eneo la Nyakaliro. Kivuko hicho kipya kinatarajiwa kutoa huduma kati ya Nyakaliro na Kisiwa cha Kome, na hivyo kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.
“Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya ukabila, dini au siasa. Sote ni watu wa Buchosa, na maendeleo ya Buchosa yanahitaji mshikamano wetu,” alisema Shigongo mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo.
Mbunge huyo aliongeza kuwa ujio wa kivuko hicho ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya wananchi, viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo, akiwataka wananchi kukitunza na kukitumia kwa uangalifu.
Aidha, aliahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mingine muhimu ya maendeleo ikiwemo barabara, afya, elimu na maji safi ili kuinua ustawi wa wakazi wa Buchosa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!