

PWANI – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 31, 2025, ameongoza hafla ya kihistoria ya uzinduzi wa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia Treni ya Umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kupitia kituo maalum cha Kwala Marshalling Yard, mkoani Pwani.
Uzinduzi huu unafungua rasmi ukurasa mpya katika sekta ya uchukuzi wa reli nchini, kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya treni za umeme, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) unaolenga kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji nchini.
Treni ya kwanza iliyozinduliwa imebeba mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Dodoma, hatua inayolenga kupunguza gharama za usafirishaji, msongamano wa malori barabarani, na kuongeza ufanisi wa biashara na uchumi wa taifa.
Kauli ya Rais Samia:
“Huu ni ushahidi kuwa tunatekeleza ahadi ya kujenga miundombinu ya kisasa. Treni hii ni mwanzo wa mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi wetu na kwa Tanzania kwa ujumla.”
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, mabalozi, sekta binafsi pamoja na wananchi waliokusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu ya maendeleo.


Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!