Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) CPA Yusuph Mwenda akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya kodi, International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD) kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa TRA katika kudhibiti ukwepaji kodi, hasa kupitia majukwaa ya kidigitali iliyofanyika leo Julia 24, 2024 katika Chuo cha Kodi (ITA), Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Profesa Isaya Jairo akizungumza katika hafla ya uzinduzi ushirikiano kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya kodi, International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD) kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa TRA katika kudhibiti ukwepaji kodi, hasa kupitia majukwaa ya kidigitali.
Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya kodi, International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD) Profesa Victor van Kommer akizungumza jambo katika uzinduzi wa ushirikiano kati ya TRA na Shirika hilo.
Afisa Uhusiano Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Bi. Oliver Njunwa akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa ushirikiano kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya kodi, International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD) kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa TRA katika kudhibiti ukwepaji kodi, hasa kupitia majukwaa ya kidigitali.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua ushirikiano na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya kodi, International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD), kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wake katika kudhibiti ukwepaji kodi, hasa kupitia majukwaa ya kidigitali kama Airbnb, Booking.com, Meta (Facebook na Instagram), na mingineyo ambayo bado hayajajisajili rasmi TRA wala kuanza kulipa kodi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Julai 24, 2025, wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Mwenda, ametoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli kupitia majukwaa ya kidigitali kujisajili rasmi na kuanza kulipa kodi, huku akiwaonya baada ya muda huo hatua kali za kisheria zitatumika, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.
“Tanzania imefungua milango ya uwekezaji kwa dunia nzima. Tuna makampuni mengi ya kimataifa yanayofanya biashara nchini. Wengine hulipa kodi, lakini yapo ambayo hukwepa, hasa yanayotoa huduma kupitia majukwaa ya kidigitali, ushirikiano huu kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wetu kubaini mianya hiyo,” amesema CPA Mwenda.
Kwa mujibu wa TRA, majukwaa ya kidigitali yanatoa huduma zinazowawezesha watu kufanya biashara kwa urahisi, lakini pia yamekuwa chanzo cha changamoto katika usimamizi wa kodi kutokana na baadhi ya watumiaji kutokujisajili wala kutoa risiti.
“Kuanzia Agosti 1 hadi 30, 2025, wafanyabiashara wote wanaopangisha nyumba kupitia Airbnb na majukwaa mengine au wanaofanya biashara za mtandaoni bila usajili TRA wanatakiwa kujisajili. Katika kipindi hicho hawatatozwa adhabu yoyote, lakini baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa,” ameongeza Mwenda.
TRA pia imetangaza kuanza kampeni maalum ya uelimishaji nchi nzima – Bara na Visiwani – kuwahamasisha wafanyabiashara wa mtandaoni kuhusu umuhimu wa kujisajili, kupata Namba ya Mlipa Kodi (TIN), na kutumia mfumo wa risiti za kielektroniki (EFD).
“Tumeweka mazingira rafiki. Tunayo App ya EFD ambayo mtu anaweza kutumia kutoa risiti moja kwa moja kupitia simu yake bila kuhitaji mashine ya gharama kubwa. Tutaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu hili,” ameeleza Kamishna Mkuu.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu watu wanaofanya biashara bila kulipa kodi ili kusaidia katika ukusanyaji sahihi wa mapato na kulinda ushindani wa haki.
“Maofisa wetu wapo katika kila mkoa. Pia tunashirikiana na taasisi kama Benki Kuu na TCRA kupitia mifumo ya malipo ili kufuatilia taarifa za wahusika,” ameongeza.
Kampeni hiyo pia imeambatana na mafunzo maalum kwa watumishi wa TRA kuhusu usimamizi wa kodi za kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya kasi ya kiuchumi duniani ambapo jumla ya wahitimu 18 wamehitimu mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti.
Kamishna Mwenda ameeleza kuwa wafanyabiashara wa mtandaoni wanaouza bidhaa kutoka nyumbani nao pia wanatakiwa kulipa kodi endapo kipato chao kinafikia angalau shilingi milioni 4 kwa mwaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA), Profesa Isaya Jairo, amesema kuwa ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kukuza uwezo wa kitaalamu wa watumishi wa TRA, hususan katika nyanja za kodi za kimataifa.
“Tunapozindua utekelezaji wa makubaliano haya, tunaweka msingi wa mafunzo endelevu, tafiti za pamoja, makongamano ya kimataifa na fursa za mafunzo kwa wataalamu wetu,” amesema Prof. Jairo.
Naye Profesa Victor van Kommer kutoka IBFD amesisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi, kutoa elimu endelevu na kujenga mazingira bora ya biashara.
Amesema kuwa kuongeza wigo wa walipakodi kutasaidia serikali kuwekeza zaidi katika elimu, afya na miundombinu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!