
Dhaka, Bangladesh – Takriban watu 27 wamethibitishwa kufariki dunia baada ya ndege ya mafunzo ya Jeshi la Anga la Bangladesh kuanguka katika eneo la chuo jijini Dhaka, Jumatatu jioni, kwa mujibu wa maafisa wa serikali. Watu wengine 88, wakiwemo watoto, wanapatiwa matibabu hospitalini kutokana na majeraha mbalimbali, hasa ya moto.
Ndege hiyo aina ya F-7 BGI, inayotumiwa kwa mafunzo ya kawaida, ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Kurmitola, ikiwa katika misheni ya kawaida ya mazoezi. Jeshi limethibitisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu ya kimitambo.
Rubani wa ndege hiyo pia amethibitishwa kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha. Serikali ya Bangladesh imetangaza siku ya kitaifa ya maombolezo, huku bendera zikiwa nusu mlingoti na sala maalum kuombwa katika sehemu zote za ibada kote nchini.
Saydur Rahman, msaidizi wa mshauri mkuu wa masuala ya afya, amesema kuwa wengi wa majeruhi walipata majeraha ya moto kutokana na mlipuko uliotokea baada ya ndege hiyo kugonga ardhi.
Jeshi la Anga limetangaza kuwa kamati maalum imeundwa kuchunguza kiini na mazingira ya ajali hiyo.
Tukio hili linatokea wiki chache tu baada ya ajali kubwa ya ndege ya Air India kuua watu 260 nchini India, ikiwemo abiria na watu waliokuwa kwenye hosteli ya chuo cha matibabu ilikokuwa imeangukia, na kuifanya kuwa mojawapo ya maafa mabaya zaidi ya anga barani Asia katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!