Mwanamke mwenye umri wa miaka 65 amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuendesha mtandao wa usambazaji wa dawa za kulevya nchini Uingereza.
Deborah Mason, anayejulikana pia kama ‘Queen Bee’, alishirikiana na wanafamilia wake saba, ambao wamehukumiwa vifungo vya kati ya miaka 10 hadi 15 kwa kosa hilo hilo katika Mahakama ya Woolwich, London.
Kundi hilo liliingiza nchini humo karibu tani moja ya kokeini katika kipindi cha miezi saba, dawa zenye thamani ya hadi pauni milioni 80 [TZS bilioni 280.3] kwa bei ya mtaani.
Mahakama hiyo imeeleza kuwa bibi huyo alitumia faida alizopata kununua bidhaa za kifahari, na pia alipanga kusafiri kwenda Uturuki kwa ajili ya upasuaji wa urembo.
Mwendesha mashtaka, Charlotte Hole amesema awali Mason aliwaajiri wanafamilia wake dada yake na watoto wake pamoja na wapenzi na marafiki wa watoto wake, kujiunga na mtandao huo, akiongeza kuwa hakutumia nguvu wala kulazimisha familia yake kujiunga na genge hilo, kwani walivutiwa na faida ya fedha alizopata.
Jeshi la Polisi la nchini humo limesema kuwa inakadiriwa kila mtu alipata zaidi ya pauni 1,000 [TZS milioni 3.5] kwa siku.
The post Bibi na familia yake wahukumiwa jela kwa kusambaza dawa za kulevya appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!