Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ameongoza mjadala maalum wa kitaaluma katika kongamano la uchumi lililofanyika tarehe 18 Julai 2025 jijini Lilongwe, Malawi. Kongamano hilo lilikuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Malawi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Dkt. Lazarus Chakwera.
Mjadala huo uliobeba mada “Kurudi kwenye Misingi: Je, kuna nafasi kwa Benki Kuu katika nchi zenye kipato cha chini kuingilia kati mfumo wa ugavi?” uliongozwa na Gavana kwa umahiri mkubwa, ambapo alisisitiza umuhimu wa kutathmini kwa kina nafasi ya benki kuu katika kusaidia ukuaji wa uchumi sambamba na jukumu lake la msingi la kuhakikisha uthabiti wa bei.
Katika hotuba yake ya utangulizi, Gavana alieleza kuwa, licha ya mageuzi yanayoendelea katika utekelezaji wa sera za fedha, kutoka kutumia mfumo unaolenga jumla ya fedha kwa kuzingatia viwango vya ubadilishaji wa fedha hadi kutumia mifumo inayojikita kwenye viwango vya riba, bado nchi nyingi zenye kipato cha chini zinakabiliwa na changamoto kubwa, hususan katika miundombinu ya kutekeleza sera hizo ipasavyo.
“Katika mazingira ambapo mfumuko wa bei unasababishwa zaidi na mishtuko ya upande wa ugavi kama ilivyo kwa nchi nyingi barani Afrika zinazotegemea kilimo ikiwemo Malawi, ni lazima tujiulize kama wigo wa jukumu la Benki Kuu unaweza kupanuliwa ili kushirikiana kikamilifu katika kukuza uzalishaji wa ndani bila kupoteza lengo msingi la uthabiti wa bei”, alisema Gavana Tutuba.
Akihitimisha mjadala huo, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa Benki Kuu haziwezi kubaki kama wasimamizi wa sera za uchumi, bali zinapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, hasa katika mazingira ambapo changamoto za kiuchumi zinahitaji ushirikiano wa taasisi zote za kiuchumi.
Kongamano hilo limejumuisha magavana wa benki kuu kutoka nchi za SADC, viongozi wa serikali, wataalam wa uchumi, wachambuzi wa sera, na wawakilishi wa mashirika ya kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kujadili changamoto na mustakabali wa sera za fedha katika nchi zenye kipato cha chini.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!