Kampuni ya Puma Energy Tanzania leo imezindua rasmi kampeni kabambe ya miezi mitatu inayoitwa “Safari ya Uhakika na Oil za Puma”, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni yao ya kitaifa ya “Twende Tanzania”. Kampeni hii inalenga kuhamasisha matumizi ya vilainishi bora vya Puma kwa wateja wote nchini, sambamba na kutoa zawadi nono kwa washiriki.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Bi. Lilian Kanora, Mkuu wa Masoko wa Puma Energy Tanzania, alisema kampeni hii ni mwendelezo wa mpango wao unaolenga kuwasogezea wateja huduma bora kwa kuwashika mkono katika kila hatua ya safari zao.

“Tunaposema ‘Twende Tanzania’, tunamaanisha kwamba tuko pamoja na mteja kila hatua ya safari yake. Safari ya Uhakika si tu kuhusu kuwafikishia vilainishi bora, bali pia kuwahakikishia wateja thamani ya matumizi yao kupitia zawadi mbalimbali,” alisema Bi. Kanora.
Kupitia kampeni hii, wateja wa Puma watakuwa na fursa ya kushinda zawadi mbalimbali kila wiki mbili kwa kipindi chote cha kampeni — kuanzia tarehe 18 Julai hadi 17 Oktoba 2025.

Baada ya kununua mafuta au vilainishi vya Puma, mteja atapokea risiti na kuchanganua (scan) QR code ili kushiriki katika promosheni. Kila wiki mbili, washindi nane watachaguliwa na kupewa vocha ya shilingi laki moja kupitia kadi ya Puma Elite, inayoweza kutumika kununua mafuta au gesi kwenye vituo vyote vya Puma nchini.
Zaidi ya hapo, mshindi mmoja mkubwa (grand winner) atapata bajeti ya mafuta ya mwaka mzima yenye thamani ya shilingi milioni tano, kama sehemu ya kuthamini uaminifu wa wateja wa Puma.

Kwa upande wake, Bw. Prosper Kasenegala, Meneja Mauzo wa vilainishi vya Puma, alieleza kuwa vilainishi vya Puma vimebuniwa kwa viwango vya kimataifa, vikiwa na teknolojia ya ODI (Oil Drain Interval) ambayo huongeza muda wa matumizi kabla ya kubadilishwa — hivyo kupunguza gharama kwa mteja na kuongeza ufanisi kwa injini.

Prosper Kasenegala (kulia), Meneja Mauzo wa Vilainishi vya kampuni ya Puma Energy Tanzania, akizungumza na waandhishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ubora wa vilainishi vya Puma wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Safari ya Uhakika na Oil za Puma” uliofanyika mwishoni wa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Lilian Kanora, Mkuu wa Masoko wa Puma Energy Tanzania.
“Tunatoa vilainishi visivyoweza kuchakachuliwa. Vinasaidia kupunguza gharama za matengenezo na kuongeza maisha ya injini — iwe ni kwa gari, bajaji, au mashine nyingine yoyote,” alisema Kasenegala.

Takwimu za mwaka 2024/25 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zinaonesha kuwa kwa sasa Tanzania hutumia zaidi ya lita milioni 60 za mafuta kwa mwaka, jambo linaloashiria ukuaji wa haraka wa sekta ya usafiri na ongezeko la mahitaji ya vilainishi bora.

Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za Puma Energy kuhakikisha wateja wake wanapata si tu bidhaa bora, bali pia thamani ya ziada kwa kila ununuzi.
The post Puma Energy Yazindua Kampeni ya “Safari ya Uhakika na Oil za Puma” kwa Wateja Wote Nchini appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!