Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Umoja Wa Mataifa Wazidi Kuliamini Jeshi La Ulinzi La Wananchi Wa Tanzania (JWTZ)

  • 39
Scroll Down To Discover

Lakabidhiwa mradi wa ujenzi wa madaraja kupitia* *MINUSCA
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kuthibitisha umahiri na uaminifu wake katika operesheni za kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa kupitia Ujumbe wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), kwa kulipatia jukumu la ujenzi wa mradi muhimu wa madaraja katika Mkoa wa Mambere-Kadei.
Ujenzi wa madaraja hayo matatu ni yale yaliyoharibika kwa muda mrefu, yakitatiza mawasiliano kati ya vijiji na miji, na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu, afya, na masoko.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Mkoa wa Equatorial, Mheshimiwa Zouketchia Emmanuel, amelishukuru JWTZ kwa kujitolea kwao na mchango wao mkubwa kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
 “Tumepata shida ya usafiri kwa muda mrefu kwa sababu ya madaraja haya. Leo tunaona mabadiliko yanayoletwa na MINUSCA kupitia marafiki  zetu wa kweli kutoka Tanzania. Asanteni sana JWTZ,” alisema Katibu Mkuu.
Naye Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mkoa wa Mambere-Kadei (ofisi ya MINUSCA, Berberati), Ndugu Landry Muketchu, amesema kuwa Umoja wa Mataifa’ umelipatia JWTZ kazi ya mradi unaotoa matokeo ya haraka (Quick Impact Project) kwa kuwa limeendelea kuonesha nidhamu, weledi na mshikamano wa hali ya juu katika kazi wanazofanya chini ya MINUSCA.
“Tumeamua kulipa JWTZ ujenzi wa Madaraja haya kutokana na ukweli kwamba limekuwa likifanya kazi zake kwa weledi wa hali ya juu kwa kila jukumu linalotolewa na Umoja wa Mataifa’ alisisitiza.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Nane cha Ulinzi wa Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, (TANBAT 08) Luteni Kanali Theophil Nguruwe, ameushukuru Umoja wa Mataifa’ kupitia MINUSCA kwa kuliamini JWTZ kwa kulipa jukumu hilo muhimu.
 “Tunaahidi kutekeleza mradi huu kwa weledi wa hali ya juu, kwa kuzingatia viwango vya Umoja wa Mataifa na kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa,” alisema Luteni Kanali Nguruwe.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walionesha furaha zao na kutoa shukrani kubwa na kukiri kuwa mradi huo ni hatua ya kweli ya kurejesha matumaini na ustawi katika maisha yao.
Mbali na mradi huu, JWTZ limeendelea kulinda amani, kutoa misaada ya kibinadamu kama vile afya, ujenzi wa shule pamoja na kushiriki michezo mbalimbali nchini humo.
MINUSCA ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2014 (kupitia azimio namba 2149) kwa lengo la kusaidia kurejesha utulivu, kulinda raia, kusaidia mchakato wa kisiasa, kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu, na kusaidia ujenzi wa Taasisi za Serikali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).



Prev Post Sakata la Rasilimali za CHADEMA: Mawakili Wadai Msajili Amepotosha Hukumu
Next Post Kudhibiti Ajali: Bodaboda na Bajaji Waja na Kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook