
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Julius K. Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Centre), limeandaa kongamano kubwa la kujadili Uchumi Jumuishi Tanzania kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kongamano hilo litafanyika Septemba 18, 2025, katika Ukumbi wa Nkrumah Lecture Theatre, Chuo Kikuu Mzumbe – Ndaki ya Mbeya, kuanzia saa 5:00 asubuhi. Lengo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili nafasi na fursa za maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Kongamano, Profesa Alexander Makulilo, amesema uhitaji wa kongamano hilo umetokana na kuzinduliwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, jijini Dodoma.
Prof. Makulilo ameongeza kuwa Rais Samia amesisitiza mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo na kushirikisha makundi mbalimbali, hususan vijana, ili kuhakikisha utekelezaji wa dira unakuwa shirikishi na endelevu.
Kongamano hilo litajadili mada kuu nne: Maudhui na Vipaumbele vya Dira 2050, Msingi wa Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, Nafasi ya Ubia katika Uchumi Jumuishi, na Uzoefu wa Sekta Binafsi kama msingi wa maendeleo endelevu.
Miongoni mwa wazungumzaji wakuu ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa; Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila; Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dkt. Gladness Salema; Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania, Dkt. Mwajuma Hamza; pamoja na wataalamu kutoka vyuo vikuu vikuu vya ndani.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!